UTANGULIZI
Katika
makala haya, nitaeleza umuundo na umuundoleo, tofauti kati ya umuundo na
umuundoleo na hitimisho.
Huwezi
kuzungumzia nadharia ya umuundoleo bila
ya kuhusisha umuundo. Kwa maana hiyo nadharia hizi huzungumziwa kwa pamoja
NADHARIA
YA UMUUNDO
Umuundo ni nadharia inayojibainisha kwa
kuangalia Ujumla wa uhusiano wa sehemu moja kwa nyingine katika kufanya kitu
kizima. Kwa mfano muungano wa maneno hufanya sentensi na sentensi zikiungana
zinaunda aya au onesho na onesho kuunda tamthiliya.
Ntarangwi, M (2004) anasema kuwa umuundo waweza
kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi miundo inayojenga
kazi binafsi.
Katika
miaka ya kwanza ya karne ya 19, mwanaisimu Ferdinard De Saussure aliyezaliwa
tarehe 26 Novemba 1857 huko Geneva, Switzerland alikuwa mwanafalsafa na
mwanazuoni wa Ki-swiss aliyejishughulisha sana na isimu, alipendekeza mtizamo
mpya kuhusu lugha. Aliiangalia lugha
kutoka mfumo rasmi hadi mfumo wa kinadharia. Kinyume na wataalamu wengine
walioshughulikia historia na sura maalum za lugha fulani, Saussure alivutiwa na
miundo inayohimili lugha zote, huku akijaribu kuonyesha kwamba lugha zote za
ulimwengu zaweza kutathiminiwa kwa kaida maalum za umuundo.
Alizua
istilahi `parole'(utendaji) na `langue' (lugha) kwa mujibu wa maelezo yake
anasema langue ni sehemu inayowakilisha welewa wetu wa uhusiano uliopo kati ya
sauti na maana . anaeleza kuwa lugha ni alama ambayo imeunganisha kati ya
kitajwa na kitaja. Kwake amesema alama ni dhana pana na ina pande mbili yaani mtajo
(kitu kilichotajwa) na kitajwa (dhana).
Kwa mujibu wa de
Saussere ‘parole’ ‘(utendaji katika lugha) huhusu msemaji kwa ujumla katika
matumizi yake au uzungumzi ni lugha katika matumizi. Kazi hii ya Saussure ndiyo iliyozaa mkondo
unaojulikana hivi sasa kama umuundo.
Muundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia
zaidi miundo inayojenga kazi binafsi.
Hata hivyo, kazi ya Saussure ilikuwa imetengewa wanaisimu peke yao.
Katika miaka ya 1950,
mtizamo huo wa Saussure ulianza kusambaa katika masomo mengine hasa wakati
mawazo yake yalipozingatiwa na Mwanaanthropolojia Claude Levi-Strauss. Kwa kuchukua maoni ya isimu ya Saussure na
kuyaingiza katika sayansi ya kijamii .
Hasa alichotaka kuendeleza dhana,
kwamba pana viwango viwili katika kuelewa maisha ya jamii, isimu, lugha na
chochote kingine kile. Viwango hivi ni
cha juu juu (surface) na cha ndani (deep).
Kwa ujumla twaona usomi wa kuitizama jamii kwa uwili unaokinzana (binary
opposition) ambao ulisambaa katika nyanja nyingi hapo baadae.
Awali ya hapo, anthropolijia ilizingatia
makundi au makabila maalum ya watu ambayo yalizingatiwa kivyao, mifumo ambayo
ilidhaniwa kwamba haibadiliki, lakini Levi-strauss alijishughulisha na mifumo
inayohimili jamii zote. Strauss alidai
kwamba pana muundo maalum ambao waweza kutumia kueleza jamii zote za ulimwengu,
kama vile ilivyo na somo la hisabu au la uchumi ambapo pana njia (formula)
ambayo yaweza kueleza maswala mengi katika somo hilio. Hapo ndipo dhana za umuundo zilipoingia
masomo mbali mbali hasa yale ya sayansi ya jamii na fasihi. Saussure alitoa maelezo ya nadharia
changamano kuhusu lugha, na ni misingi ya nadharia zake inayotoa nguzo ya mbinu
za umuundo, ( Ntarangwi, 41: 2004).
Ingawa huwa tunatumia
lugha kuzungumza kuhusu maisha, Saussure hakulizingatia jambo hilo bali
alisisitiza kwamba lugha ni kiungo kamili kinachojisimamia. Kwamba ni kiungo kilicho na masharti na
sheria zake. Hivyo basi kuwepo kwa vitu
duniani hakuathiri aina ya lugha iliyopo.
Isitoshe, alidhamiria kudai kwamba lugha kwa kujisimamia haibadiliki
wala vipande vyake haviathiriwi na mabadiliko yoyote ya kijamii.
Katika mkabala huo,
neno ni ishara huru inayoelezwa kwa kutofautishwa na nyengine. Lugha ni mfumo wa uhusiano kati ya viungo
kadhaaa vinavyoijenga; ni muundo, sio kitu.
Dhana hii yaweza kueleweka zaidi tukizingatia maneno ya Saussure ya
`kionyeshi' na `kinachoonyeshwa'. Neno
katika lugha ndilo `kionyeshi' na dhana inayorejelewa ni neno hilo ndiyo
`kinachoonyeshwa'. Kwa mfano neno mtoto ndio kionyeshi picha ya mtoto
kama kirejelewa ndio kinachoonyeshwa.
Vyote viwili haviwezi
kutenganishwa, lakini umuundo hujishughulisha zaidi na uhusiano wa vionyeshi na
jinsi vinavyofanya kazi kuliko kuangalia nje ya mfumo wa lugha, yaani kinachoonyeshwa. Kwa msingi kabisa, Saussure alizingatia zaidi
mpangilio wa ndani wa lugha, ule muundo wake na sio mahusiano ya vipande
vyake. Wahakiki wanooegemea mkondo wa
Saussure huzingatia kwamba matini husika ni mfumo unaojisimamia na hivyo basi
huwa hamna haja ya kutumia mambo ya nje ili kuhakiki kazi ya fasihi. wahakiki huzingatia matini kama kiungo kamili
kinachoweza kuhakikiwa kivyake. Hivyo
basi mhakiki wa umuundo hujaribu kuweka sarufi ya matini pamoja na sheria za
jinsi matini hiyo hufanya kazi. Mhakiki
anayezingatia zaidi muundo wa lugha ya matini bila shaka hupuuza dhana ya jadi
kuhusu kile matini hiyo huweza kutueleza
kuhusu maisha; na hivyo basi hufanya mtindo wa kazi yenyewe kiini cha uhakiki
wake.
Kwa hivyo wahakiki
wanaotumia nadharia ya umuundo hujaribu kuzingatia matini pekee huku wakiepuka
kuifasiri kazi ile kulingana na kaida zilizowekwa kuhusu jinsi matini hufanya
kazi. Hata hivyo, huenda njia hii isiwe
ya kufaa sana kwa sababu huwa inachukulia kwamba kila kitu kimeundwa katika
mpangilio halisi usiotatanika na usiotegemea mambo mengine yaliyo nje
yake. Ama kwa hakika, hata lugha yenyewe
haiwezi kabisa kufanya kazi bila kuathiriwa na mambo mengine kama vile
mazingira yake
Wakakiki wa muundo
walichunguza upatanishi wa sauti, kiimbo, arudhi na utunzi wa maashairi
wanaamini matini ya kifasihi huwa na viwango mbalimbali. Mhakiki anachunguza
vipengele hivi kwa viwango tofauti tofauti.
Mkondo huu wa mawazo ya umuundo kuhusu sayansi
za jamii ulianzia ulaya na kuathiri mtazamo wa elimu mbalimbali (duniani) kama
vile: Falsafa, Anthropolojia, Historia, Uhakiki wa kifasihi na Sasiolojia.
Kwa hivyo twaweza kuangalia jamii katika muundo
wake wa kijuu juu na kuielewa lakini tukitaka kupata maana mwafaka lazima
tuchunguze muundo wake wa ndani ambao hupatikana katika kila jamii ya wanadamu.
Kwa hiyo hata katika kuielewa fasihi lazima tuifahamu lugha yake.
Katika kupata maana
lazima kuwe na uhusiano wa kipembetatu yaani kuna DHANA, ALAMA na KITAJWA.
Upungufu wa nadharia hii ndiyo uliochochea
kuzuka kwa Umuundo- mpya.
NADHARIA
YA UMUUNDOLEO
Umuundoleo
hutumiwa kuelezea mikabala ya uhakiki iliyozuka kuyapinga au kuyaendeleza
mawazo yaliyokuwa kwenye umuundo.
Tunatumia
neno Umuundoleo kuonyesha mtizamo wa kimuundo katika fasihi ambao ulitokea
baada ya Umuundo. Japo dhana hii haiwezi
kupewa maana moja maalum, imehusishwa na maendeleo kutoka au katika kazi za
Derrida (1973, 1976), Lacan (1977), Kristeva (1981, 1984, 1986), Althusser
(1971) na Foucault (1978, 1979a na b, 1981, 1986). Kazi hizi nazo zilichangiwa na kazi za
Ferdinand de Saussure na Emile Benveniste (kuhusu isimu-jamii ya umuundo), kazi
ya umarx hasa kupitia nadharia ya itikadi iliyoendelezwa na Louis Althusser, na
kazi ya tathimini-nafsi ya Sigmund Freud na Jacques Lacan.
Kazi
hizi zimetoa athari mbali mbali kwa nadharia tofauti lakini zote zinazingatia
makisio sawa kuhusu lugha, maana, na ubinafsia (subjectivity). Lugha
yachukuliwa kama nguzo maalum ya uainishi wa mpangilio wa jamii, maana za
kijamii, nguvu na urazini wa kibinafsi.
Hii ni kwa sababu ni katika lugha ambapo maana za mpangilio wa jamii na
matokeo yake ya kisiasa na kijamii hujengwa na kupingwa.
Ni kupitia lugha ambapo hisia na maana yetu ya
kibinafsi (ambayo inatufasili) hujengwa.
Aidha, lugha haielezi ubinafsi wa kipekee wa mtu bali hujenga ubinafsia wa
mtu kwa njia zilizojengeka katika miundo ya jamii yake. Katika Umuundo-leo, ubinafsia sio hali yenye
umoja au isiyobadilika, bali hubadilika kila mara ili kuchukuana na hali halisi
ya kihistoria na kisiasa ili kudumisha nafasi ya mhusika katika jamii.
Umuundo-leo,
kama nadharia nyinginezo ina makisio fulani kuhusu lugha, ubinafsia, ufahamu,
na ukweli. Nguzo zake, ambazo zatokana,
kama tulivyotaja hapo juu, na mwanaisimu wa kiimuundo Ferninard de Saussure, ni
kwamba lugha, badala ya kudhihirisha uhalisi wa kijamii uliopo, huwa yatujengea
uhalisi huo wa kijamii. Kwa hivyo sio
uhalisi wa kijamii wala ulimwengu asilia huwa na maana zinazodhihirishwa ni
lugha. Lugha mbali mbali pamoja na
matumizi mbali mbali ya lugha moja huugawa ulimwengu na kuupa maana kwa njia
tofauti ambazo haziwezi kupatana ili kuunda kigezo kimoja kinachodhihirisha
uhalisi wa jamii. Kwa mfano, maana ya
tajiri hutofautiana katika lugha mbali mbali na hata kati ya miundo tofauti ya
lugha moja, na hutegemea matumizi na muktadha wa matumizi hayo. Ndipo sasa hapana maana moja ya neno au fungu
la maneno.
Miundo
yote ya umuundo-leo huchukulia kwamba maana hujengwa katika lugha na huwa yule
anayezungumza lugha hiyo hawezi kuhakikisha maana hiyo. Kwa hivyo tofauti na maoni ya Saussure, maana
huzaliwa na kuundwa kwa njia mbali mbali.
Hata
hivyo nadharia hii hukubaliana na wazo lake kwamba lugha haimuliki maana; bali
maana hukuzwa katika lugha na kwamba ishara hazina maana ya kivyake bali hupata
maana katika mkururo wa lugha pamoja na tofauti yake na ishara nyingine. Dhana hii ni muhimu sana kwa sababu
yadhihirisha lugha kama chombo cha kijamii ambacho chapingwa na kung'ang'aniwa.
Kulingana na nadharia hii basi, neno 'mama'
kwa mfano, huwa halina maana ya kindani inayotokana na lugha husika bali huwa
na maana za kijamii zilizotokana na lugha hiyo na ambazo zinakinzana na
kubadilika kulingana na mazingira na kipindi cha kihistoria.
Kwa
hivyo kinyume na maoni ya wanamuundo kama vile Levi-Strauss walioshikilia
kwamba maana ya kisa, kwa mfano, ipo katika matini na maana hiyo hiyo hutokea
katika matini nyengine yoyote, nadharia hii yaeleza kuwa maana ya kisa ni amali
ya msomaji/msikizi (hadhira) na kwamba pana fasili mbali mbali za kisa hicho
kulingana na muktadha. Hivyo basi kwa
umuundoleo twaweza kueleza kuwepo kwa wingi wa maana pamoja na mabadiliko yake
kwa kuona maana sio kama iliyojengwa katika ishara zisizobadilika bali kama
iliyo katika viashiria (signifiers) ambapo kiashiriwa (signified)
hubadilikabadilika. Hapo ndipo
alipojikita Derrida ambaye aliingiza
dhana
ya muktadha katika kueleza maana katika lugha na matini. Wahakiki wanaozingatia nadharia hii basi
huongozwa na dhana ya kubadilika kwa maana katika miktadha mbali mbali na hivyo
basi kuwashurutisha kuzingatia muktadha wa kazi hiyo kama nguzo ya kueleza kazi
hiyo. Mtaalamu huyu anazuka na dhana maarufu ya utofauti (difference), kwa
maoni yake maana hutokana na mikakati au mbinu mbili muhimu, ‘tofauti’
(difference) na ‘uahirisho’ Wamitila (2002:179 ) anaiita kuwa ni tofahirisho ambalo linafumbata
dhana mbili hizi.
Wanamuumo
wanaangalia muktadha wa kiusemi au kimazungumzo na huweza kubadilika kutegemea mukatadha wa kiusemaji. Ikiwa muktadha wa kiusemi
utabadilika maana nayo inabadilika.
TOFAUTI
KATI YA MUUNDO NA UMUUNDOLEO
Kwanza,
Nadharia ya umuundo imeeanza karne ya 19 na mawazo yake yanatokana na falsafa
ya ya de Saussure na Levi Strauss, nadharia hii ya mwanzo na inalenga katika
kuonesha namna mfumo wa lugha ulivyo na jinsi unavyotoa maana ya kitu na
matini. Wakati nadharia ya wanamuundoleo
imeanza karne ya 20 ilijikita kwa Jacque Derrila na inalenga zaidi katika kuonesha
namna maana inayopatikana. Husisitiza maana hutokana na jamii au mazingira.
Wanamuundo
hawatilii mashaka uwepo wa uhalisia yaani baadhi ya vitu, binaadamu au jamii ni
uongo tu ni mawazo tu, vitu vyote ambavyo viko katika mazingira havina uhalisia
wowote, kwa mujibu wa nadharia hii, wandishi wa vitabu wanachokiandika katika
vitabu vyao vya fasihi havina uhalisia wowote katika mazingira halisi. Wakati wanamuundoleo wao wanaona kuwepo
kwa uhalisia, na dhana au mawazo ni vitu viwili tofauti, hupatikana kulingana
na mazingira kila mtu na ukweli wao, wao hawachanganyi kati ya uhalisia na
dhana yenyewe wanaona ni vitu tofauti.
Pia,
wanamuundo wanaisitiza uhusiano wa mazingira na maana kutengenezwa, wao
huangalia maana kuwa ni kitu cha kutengenezwa, yaani mazingira hutengeneza
maana,wao uona ulimwengu wa nje ni wa kiurejelezi mhakiki atahakiki kwa
kurejelea jamii yake, kwa mujibu wa nadharia hii katika kazi ya fasihi kuna
mambo mengi ambayo mwandishi ameandika, mhakiki wa kazi ya fasihi uhakiki kwa
kungalia mazingira yake na kufanya uhakiki kulingana na mazingira yake, kwa
mfano katika kitabu cha kivuli kinaishi
( uk 24-25) kumezungumziwa kukithiri kwa rushwa katika jamii Giningi, watu
wanatoa na kupokea rushwa, mhakiki ataitazama jamii yake kama swala la rushwa
katika mazingira yake ni swala linalokwamisha maendeleo ataitafsiri maana
kulingana na jamii yake ndicho anachokirejelea. Atasema kuwa rushwa hukwamisha
maendeleo ya jamii yetu, mhakiki atapendekeza kuwa ili tuweze kujenga jamii
mpya yenye kufuata haki na usawa hatuna budi kupiga vita rushwa, kwa mhakiki
ambaye rushwa ktika jamii yake si tatizo hawezi kusema ni kikwazo cha maendeleo
badala yake atazungumzia kama jamii yake inavyoichukulia lugha . Wakati kwa upande wa nadharia ya
umuundoleo wao wanasema:
Mazingira
na maana hazina uhusiano kwakua hutokea utata katika uumbaji wake, uwepo wa
mifumo mingi husababisha utata yaani kinachoelezwa na lugha huwa hakipo kwa
maana kwamba hakirejelei kitu kilicho nje yake, kwa mujibu wa nadharia hii
mhakiki atahakiki kazi ya fasihi bila kuhusiasha jamii, atasoma kitabu na
kuhakiki kwa mawazo yake yeye mwenyewe ili kuondoa utata katika kutoa maana,kwa
mfano kwa kitabu cha kivuli kinaishi mhakiki
atakiangalia bila kuangalia jamii yake.
Tofauti
nyingine ni kwamba, mfumo wa mazingira hujenga fikra na kuleta maana, watu
wenye mazingira sawa huchukulia vitu sawa yaani mfumo hujenga mpaka wa maana,
wanamuundo huangalia mfumo wa maisha ukoje na kutoa maana ya kitu kulingana
mfumo wa maisha ukoje, kwa mfano katika tamthilia ya Ngoswe - Penzi kitovu cha uzembe kilichotungwa na E. Semzaba
anaelezea ndoa za mitaala katika familia ya
balozi Ngengemkeni, mhakiki au msomaji wa tamthilia hii kwa kuwa fikra
yake iliyojengeka kutokana na mazingira yake atasema kuwa ndoa za mitaala zinaathari kuwa watoto
hawapati malezi bora kutokana au wanawake hawana upendo.
Wakati wanamuundoleo
wanasema hakuna maana moja, kuna maana nyingi dhana moja hujenga maana nyingi
yaani mfumo kuibua maana nyingi, kwa mujibu wa wanamuundo baada ya uandishi wa
kitabu kila mhakiki au msomaji wa kazi ya fasihi atakuwa na maana yake katika
kuichambua kazi husika ya fasihi, hakuna maana moja kwa mfano wa methali samaki
mkunje angali mbichi atakae sikia methali hii anaweza kusema kuwa
samaki anatakiwa kukunjwa akiwa mbichi lakini maana ya methali hii ni mtoto
anatakiwa afundishwe akiwa bado mdogo pia anaweza akaja mwingine kwa maana nyingine kulinganana na dhana
husika, kwa maana kwamba lugha ina uwezo mkubwa wa kuzaa maana.
Wanamuundo
wanarahisisha maana, na kuonesha vielelezo muhimu kuonesha maana moja, wao
uhusisha maana ya vitu mbalimbali kuwa moja, kwa mfano ulevi na utapeli
uhusisha kuwa ni uovu, uangalia uhusiano wa maana, kwa mfano katika fasihi
waandishi wa vitabu tofauti tofauti wanaeleza mambo mbalimbali ambayo wahakiki
au wasomaji uhusisha na kuwa ni dhamira moja, katika riwaya ya watoto
wa mama ntilie iliyotungwa na Emmanuel Mbogo riwaya imezungumzia maisha
ya walalahoi, katika riwaya hii mwandishi amehusisha mambo yote na umasikini na
kuoana dhamira kuu ni umasikini. Wakati
wanamuundoleo wao wanadai kuwa kila kitu kielezewe kwa upekee, wanafikiria kuwa
tofauti walizoziondoa zina umuhimu na zinaziba mapengo, kwahiyo kuhusisha maana
kwao ni kuweka mapengo kila kitu kiongelewe kwa upekee wake.
Tofauti
njingine ni kwamba, wanamuundo wanaangalia ukweli ambao utamgusa kila mtu yaani
kufuata muundo mmoja, kwao lugha zote zina muundo wa jumla yaani
kitakachochambuliwa Zanzibar ndicho kitakacho patikana mtwara, Jamii nzima
itakuwa inahusika na jambo hilo kwa mfano maswala ya ukimwi, rushwa na mapenzi.
Wanamuundoleo
wao hawakuonesha ukweli wa kimajumui na kuangalia vitu ambavyo vinatutenganisha
kila mmoja na muundo wake na kuaangalia kipi kinatufanya tuwe tofauti, wao
huuangalia utofauti ambao upo katika jamii husika , utofauti katika mila na
desturi mbalimbali za jamii ,kwa mfano jamii moja inaendeleza mila na desturi
za kukeketwa mwandishi ataangali utofauti huo kwa jamii nyingine ambayo haina mila
hizi.
Vilevile,
Wanamuundo hutilia mkazo zaidi kwenye muundo, muundo ndio hutengeneza fikra kwa
mfano katika tamthilia, riwaya na ushairi au kazi mbalimbali wanamuundo huangalia
muundo wa kazi hizi, wakati wanamuundoleo wanaangalia kuwa mazingira ndio
huleta mpaka, huangalia lugha kwenye mazingira ndio hutengeneza fikra zetu,
binaadamu ni wabunifu mipaka huwekwa na mfumo, kwa mfano uhakiki wa kitabu cha
riwaya ya kusadikika ya Shaaban Robert ulivyofanywa kipindi cha miaka
ya nyuma ni tofauti na mhakiki anayehakiki kazi ya fasihi ya mwandishi huyo kwa
sasa.
Wanamuundo
kama vile Levi-Strauss anaona maana ya kisa ipo katika matini na maana hiyohiyo
hutokea katika matini nyingine yoyote, anahusisha maana moja tu ya kisa na
maana nyingine, kisa kimoja na kingine hufanana kimaana wakati wanamuundoleo wao maana ya kisa ni mali ya msomaji au
msikilizaji na kwamba pana fasili mbalimbali ya kisa kulingana na kisa, msomaji au msikilizaji
atatoa maana kilingana na muktadha na kusababisha kutoakea maana pana, kwa
mfano katika riwaya ya mfadhili
iliyotungwa na Hussein Tuwa, msomaji anaweza kuongelea kuwa riwaya hii
imeelezea maswala ya mapenzi lakini pia msomaji mwingine anaweza kuielezea kwa
maneno mengine na kutoa maana nyingine.
Kwa
ujumla Umuundo wamejikita zaidi katika dhana moja, kwamba mfumo wa maana ni
jinsi unavyofanya kazi, maana ya kazi ya inatokana na sheria na kaida
mbalimbali za mifumo tofauti ya kuashiria. Maana haitokani na mtu ( mwandishi
au msomaji). Wakati Umuundoleo unaishia kumpuuza mwandishi na kuishusha hadhi
kazi ya fasihi kwa kutia mkazo mkubwa kwenye msomaji wa kazi hiyo. Wanajikita
zaidi kwamba mzungumzaji au msomaji ndio wanaongoza mfumo. Nadharia zote mbili
zina kamilishana mapungufu ya nadharia ya umuundo ndio yalianzisha umuundoleo.
asante kwa kazi yako imejitosheleza saana
JibuFutawatu kama nyie ndiyo wana leta maendeleo ya kweli
Kazi nzuri kiukweli pongezi ni yako bila makunyanzi endelea kutuelimisha mola akutangulie katika kazi zako
JibuFutaKazi nzuri msomi wa lugha ya kiswahili.... Asante kwa kupanua mawazo ya wasomi wa lugha kwa jumla
JibuFutaAsante naungana na wewe ushauri tukazane katika utafiti zaidi ili tufikie malengo Asante
FutaMatini ni nzuri inaeleweka hivyo ni vyema tukawa na mfumo mzuri wa kufanya utafiti zaidi juu ya nadharia hizi ili tupate ushahidi wa kutosha juu ya nadharia husika
JibuFutaKazi Safi sn iko vzr
JibuFutaKazi nzuri imefafanuliwa vyena nauliza jee huu umuundo mpya ndio unaoitwa semiotiki?
JibuFutaKazi nzuri sana nimeongeza maarifa
JibuFutaUmejaribu kueleza ukweli na kurahisisha kuzijua nadharia hizi ambazo zinaonekana ngumu KATIKA uhakiki wa fasihi
JibuFutaKazi mzuri zaidi.Imenipa maarifa Tosha .
JibuFutaKazi mzuri.
JibuFutaKazi nzuri.
JibuFutaStainless steel vinoids - Titanium Glass Art
JibuFutaThis titanium bar stainless steel titanium vs steel vinoids glass titanium flask art project is a unique collaboration between the Art of Professionalism ecm titanium and Engineering. The piece will allow the Art of titanium mokume gane Professionalism